GULAMALI AANDIKA HISTORIA ILONGERO: MKATABA WA UJENZI DARAJA LA MGORI WASAINIWA

Mbunge wa Jimbo la Ilongero, Haiderali Hussin Gulamali, ameandika historia leo tarehe 3/03/2026 baada ya kushuhudiwa rasmi utiaji wa saini wa mkataba wa ujenzi wa Daraja la Mgori – mradi utakaotekelezwa ndani ya miezi 8 kuanzia sasa.
Na Abdul Ramadani Sigida Tanzania
Hatua hiyo imekuja ndani ya siku 100 tangu kuapishwa kwake, ikiwa ni matokeo ya juhudi zake za haraka na za kimkakati. Ndani ya siku 30 tu baada ya kuwa mbunge, aliwaongoza baadhi ya madiwani kwenda kuonana na Waziri wa TAMISEMI, Riziki Shemdoe, kuwasilisha changamoto zinazowakabili wananchi wa Ilongero, ikiwemo tatizo sugu la korongo la Mgori.
Kwa muda mrefu, korongo hilo limekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za kijamii na kiuchumi, huku likihatarisha maisha ya wananchi wakati wa mvua kwa kusombwa na maji. Wakati mwingine wananchi walilazimika kusubiri hadi saa 8 ili kuvuka kwenda upande wa pili – hali iliyokuwa inarudisha nyuma maendeleo ya jimbo hilo.
Kutokana na ufuatiliaji wa karibu wa Mbunge Gulamali pamoja na ushirikiano mzuri na Wizara, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekubali kutenga zaidi ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo muhimu.
Ujenzi wa Daraja la Mgori ni ushahidi wa uongozi wa vitendo, unaoweka mbele maslahi ya wananchi. Ni ishara ya matumaini mapya kwa wakazi wa Ilongero – kwamba changamoto zikisemwa kwa ujasiri na kufuatiliwa kwa bidii, hupata ufumbuzi.
Hakika, huyu ndiye Gulamali (Basima) – kimyakimya lakini vitendo vinaonekana. Kazi na utu, Ilongero tunasonga mbele
Na Abdul Ramadani Sigida Tanzania
Comments
Post a Comment